Mabaki yaliyopatikana Pemba nchini Tanzania ni ya shirika la Malaysia Airlines iliyotoweka mwaka 2014
Mabaki ya ndege yaliyopatikana
katika pwani ya visiwa vya Pemba nchini Tanzania yalitoka kwa ndege ya
shirika la Malaysia Airlines iliyotoweka mwaka 2014, maafisa wa Malaysia
wamethibitisha.
Waziri wa uchukuzi wa Malaysia Liow Tiong Lai
amesema kupitia taarifa, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters,
kwamba baada ya uchunguzi imebainika kwamba kipande hicho kikubwa cha
bati kilichopatikana mwezi Juni ni cha ndege hiyo safari nambari MH370.
Amesema
uamuzi huo ulifikiwa na wataalamu kutoka Idara ya Usalama wa Safari za
Ndege ya Australia (ATSB) na wale wa kuchunguza usalama wa MH370.
Mabaki
hayo pia yalikuwa na muhuri wa kuonesha tarehe ya kuundwa kwake ambayo
ilikuwa Januari 23, 2002. Ndege hiyo ya Malaysia iliwasilishwa kwa
shirika hilo 31 Mei, 2002, kwa mujibu wa tovuti ya shirika la Channel
News Asia.
Ndege
hiyo aina ya Boeing 777 ilitoweka Machi 2014, ikiwa na abiria 239 baada
ya kupaa kutoka Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia kuelekea Beijing.
Bw
Liow amesema mabaki hayo yatachunguzwa zaidi kubaini iwapo kutapatikana
ufumbuzi kuhusu kilichotokea hadi ndege hiyo ikatoweka.
Mabaki mengine yanayodhaniwa kutoka kwa ndege hiyo yamepatikana Msumbiji, Afrika Kusini na visiwa vya Rodrigues, Mauritius.
CHANZO BBC SWAHILI
CHANZO BBC SWAHILI


Post a Comment